Siku
moja baada ya majambazi kuvamia Benki ya Access Tawi la Mbagala Rangi
Tatu, kuua watu watatu akiwamo Polisi na kujeruhi watu wengine watatu
akiwamo polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga amesema
wataomba msaada wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ili kukabiliana na matukio
ya ujambazi.
Alisema Jeshi la Polisi linajipanga upya kuhakikisha wananchi wanakuwa na amani kwa kuwashughulikia majambazi popote walipo.
Waziri
Kitwanga alisema wanaanza na Mkoa wa Pwani, kwa kuhakikisha wanawasaka
na kufyeka mapori yote ya Bagamoyo na kwingineko ili kuvunja mtandao
wao.
“Kama
walidhani Jeshi la Polisi limelala lipo macho, walichofanya ni kama
wamemuamsha aliyelala, tutawasaka, tutawakamata na tutawapeleka kwenye
mkono wa sheria na tutahakikisha tunawamaliza wote,” alisema Kitwanga.
Alisisitiza
kuwa wanaotumia pikipiki nguvu ya ukaguzi itaongezwa dhidi ya vyombo
hivyo, kwa sababu inaonekana wahalifu wengi hasa majambazi hutumia
usafiri huo kutekeleza uovu wao.
Akielezea
tukio la uporaji wa Mbagala, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Simon Sirro alisema wamefanikiwa kuwaua majambazi watatu kati ya
12 waliofanya uvamizi huo.
Alisema
majambazi hao walikufa baada ya kupigwa risasi katika majibizano ya
risasi na Polisi katika Kijiji cha Chui Mkuranga, baada ya kujaribu
kutoroka walipozidiwa nguvu.
Alisema
majambazi hao wakiwa na pikipiki sita, huku kila moja ikiwa na
majambazi wawili waliokuwa na bunduki aina ya SMG na mabomu ya kutupa
kwa mkono, walivamia benki hiyo na kuwashambulia kwa risasi kisha
kuwajeruhi wafanyakazi wa benki hiyo waliokuwa katika chumba cha
kuhifadhia fedha.
Aliwataja
waliojeruhiwa kuwa ni Salum Juma na Francis Amani, na kupora kiasi cha
fedha kinachokadiriwa kuwa kati ya Sh20 na 30 milioni za kaunta baada ya
kushindwa kuvunja chumba cha kuhifadhia fedha.
Alisema
kabla ya kuingia ndani, walivamia kibanda cha walinzi na kumpiga risasi
askari mwenye namba H7739PC Khalid Juma ambaye alifariki dunia papo
hapo.
Pia,
walimjeruhi kwa kumpiga risasi kwenye nyonga askari Shaban, ambaye
amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili na kupora bunduki mbili.
Kamanda
Sirro alisema majambazi hao baada ya kufanya uporaji walipokuwa
wanaondoka, walifyatua tena risasi iliyompata kidevuni na kumuua papo
hapo Abdi Salum, ambaye ni muuza duka jirani na benki hiyo na Baraka
Fredrick, mlinzi wa kampuni ya Security Group of Africa.
“Hata
hivyo Polisi wamefanikiwa kukamata bunduki tatu kati ya hizo mbili ni
mali ya Polisi, mabomu matatu ya kutupa kwa mkono na pikipiki sita
zilizokuwa zikitumiwa na majambazi hao walipozidiwa nguvu walizitelekeza
na kukimbia,” alisema Sirro.
Katika
hatua nyingine, Februari 18, eneo la Kiwalani polisi walikamata
majambazi watatu wakiwa na bastola moja na Februari 24 eneo la Upanga
karibu na Daraja la Sarender, askari waliwakamata watuhumiwa watatu kwa
makosa ya kujihusisha na ujambazi wa kutumia silaha.
Kamanda
Sirro alisema baada ya kuwahoji walikiri kufanya matukio ya ujambazi wa
kutumia silaha na kumtaja mtuhumiwa mwenzao mmoja anayeishi Tabata
Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
“Alipofuatwa nyumbani kwake, alikutwa na sare za jeshi hilo, redio ya upepo na pingu,” alidai kamanda huyo.
0 comments:
Post a Comment