Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii katika serikali ya awamu ya nne,
Ezekiel Maige, jana alitajwa katika kesi inayomkabili aliyekuwa
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bernard Murunya
ambaye ameshitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi.
Katika kesi hiyo, Maige anadaiwa kulipiwa nauli ya safari ya nje na
mamlaka hiyo kwa idhini ya Murunya, ambaye sasa ni Mbunge wa Afrika
Mashariki.
Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Sezari Semfukwe, alidai kuwa Murunya
na aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Mamlaka hiyo, Shad
Kiambile, waliidhinisha malipo ya dola 66,890. Alidai kuwa fedha hizo
zilikuwa kwa ajili ya safari ya Maige na msaidizi wake aliyetajwa kwa
jina la E. Muyungi na Murunya mwenyewe.
Semfukwe, ambaye ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa mamlaka hiyo, alidai kuwa
Murunya na Kiambile, ndio walioidhinisha madokezo kwa ajili ya malipo
hayo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Hamidu Sembano, akisaidiana na Rehema
Mteta, mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia
Kisinda, Semfukwe alidai kuwa utaratibu wa maombi ya safari, unatokana
na maelekezo ya mkuu wa idara na kujaza fomu inayoonyesha anakwenda wapi
na kwa muda gani.
Sambamba na hilo, alidai kuwa aina zingine za safari zinahusisha watu wa
nje ambao, si waajiriwa wa NCAA kwa dokezo la mkuu wa idara au shirika.
Alidai kuwa alitoa hundi ya malipo namba 309/0238 ya Septemba 9/2011,
ambayo ilikuwa na dokezo la safari kutoka kwa Murunya kwenda kwa Mkuu wa
Kitengo cha Fedha. Pia alitoa hundi ya malipo nyingine iliyokuwa
ikionyesha imelipwa dola zaMarekani 66,890 kwa kampuni ya Wakala wa
Usafirishaji ya Cosmas.
Aliendelea kudai kuwa hundi za malipo namba 310/0379 ya Oktoba 29, 2011
na ankara namba 5609 ya Septemba 7, 2011 zililipwa kwa Antelope Tours
& Traveling kwa ajili ya tiketi za Murunya, Muyungi na Maige kwa
malipo ya dola za Marekani 66,890 (zaidi ya Sh. milioni 133).
Shahidi hiyo alidai kuwa kumbukumbu ya kitabu cha malipo ya hundi
inaonyesha hundi namba 002758 na 002755 za Septemba 9, 2011 zililipwa
kwa kampuni ya Cosmas Travelling Agent na zilitiwa saini na Kiambile na
Murunya.
Hata hivyo, wakati shahidi huyo akitoa vielelezo hivyo mahakamani hapo
ili vitumike kama ushahidi, malumbano ya kisheria yaliibuka baina ya
mawakili wa pande zote.
Malumbano hayo yaliibuka baada ya upande wa washtakiwa, ukiongozwa na
wakili Amani Mirambo, kutaka kujua ni vielelezo vingapi au vya aina gani
ambavyo upande wa mashtaka unavileta.
Hatua hiyo ilisababisha malumbano ya kisheria hivyo kumfanya hakimu
kuahirisha kesi kwa dakika 10. Baada ya muda huo, alirejea mahakamani
baada ya dakika hizo na kuwahoji.
Baada ya kuhoji pande zote mbili, kutokana na malumbano ya kisheria,
Hakimu alikatizwa na Wakili wa Serikali Hamidu Simbano, aliyemwomba
kuahirisha kesi hiyo na kutaja tarehe nyingine ya washtakiwa kusomewa
maelezo yao ya awali.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Rehema Mteta, aliwasomea maelezo ya awali juu ya tuhuma za
matumizi mabaya ya madaraka yaliyosababisha mamlaka hiyo kupoteza dola
66,890 (Sh. 133,780,000).
Mteta aliwataja washitakiwa, mbali na Murunya na Kiambile, kuwa ni
Meneja Utalii wa mamlaka hiyo, Veronica Funguo na Salha Issa ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Cosmas Travelling Agent.
0 comments:
Post a Comment