Top Ad 728x90

Tuesday, 1 March 2016

Umeya wa Dar Utamponza Magufuli...Bado Chama Chake Hakijawa na Dhamira ya Kweli ya Kutaka Mabadiliko

Siku chache baada ya Mhe.John Pombe Magufuli kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuanza "kutumbua majipu" rafiki yangu mmoja ambaye ni mwandishi wa gazeti moja la kila siku aliniambia hii ni nguvu ya soda.

Alisema Magufuli anaweza kuwa na dhamiri ya kweli ya kufanya mabadiliko lakini atakwamishwa na chama chake. Bado chama chake hakijawa na dhamira ya kweli ya kutaka mabadiliko. Hata majipu anayotumbua kuna mengine hayatumbuliki maana yanagusa uhai wa chama chake.

Aliifananisha dhana ya "kutumbua majipu" na "kuvua gamba" ambayo ilitumika na chama cha mapinduzi miaka kadhaa iliyopita kama ajenda ya kupiga vita ufisadi. Lakini ajenda hii ilishindwa kuvua hata gamba moja ndani ya chama hicho licha ya kupigiwa chapuo na viongozi wakuu wa chama hicho.

Kwahiyo dhana ya "utumbuaji wa majipu" ni sawa na "uvuaji gamba". Kuna majipu hayawezi kutumbulika hata kama Rais Magufuli ana dhamira ya kufanya hivyo.

Moja ya jipu kubwa kabisa ambalo lipo usoni kwa Magufuli na amelikalia kimya kama hajaliona ni suala la umeya wa Jiji la Dar es Salaam. Hili ni jipu ambalo Magufuli ameshindwa kulitumbua na haoneshi kuwa na mpango huo.

Tangu uchaguzi mkuu ufanyike na wananchi kuchagua wabunge na madiwani yapata miezi minne sasa. Katika kipindi hiki cha miezi minne jiji la Dar es salaam ni kama limesimama.

Jiji halina Meya, hakuna kamati za halmashauri, hakuna mipango ya maendeleo, hakuna vikao vya madiwani, jiji limesimama kwa sababu ya mvutano wa kisiasa kati ya CCM na Muungano wa vyama vya UKAWA juu ya nafasi ya Umeya.

Mvutano huu umesababishwa na CCM kutokubali kuachia madaraka ya kuongoza jiji la Dar kwa vyama vya upinzani. Bado haijajulikana hofu ya CCM inatokana na nini lakini hadi sasa wamefanya mbinu mbalimbali kuhakikisha wanahujumu uchaguzi wa Umeya wa Dar na kuweza kuongoza tena jiji hili.

Baadhi ya mbinu zilizotumika ni pamoja na kutumia wabunge wa viti maalumu kutoka Zanzibar ambao baada ya mvutano mkubwa wa kisheria walizuiwa kupiga kura ya kumchagua Meya.

Lakini watu wanahoji kwanini CCM walete wabunge wa Zanzibar kuja kupiga kura Dar? CCM walijua kuwa wabunge wa Zanzibar hawana uhalali wa kisheria wa kupiga kura bara lakini wakalazimisha. Kwanini?

Baada ya wabunge hao kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo CCM hawakuridhika. Wakabuni mbinu nyingine ya kuwatumia Mawaziri walioteuliwa kuwa wabunge kabla ya kuapishwa. Hilo nalo likakumbana na kizingiti cha kisheria.

Hatimaye uchaguzi ukaitishwa tena tarehe 05 mwezi February mwaka 2016 lakini Chama cha mapinduzi kikakimbilia Mahakamani kuweka zuio la kuahirisha uchaguzi huo. Kwahiyo wajumbe wakafika ukumbini na kutangaziwa kuwa uchaguzi huo umeahirishwa.

Hatimaye uchaguzi huo ukaitishwa tena kwa mara ya nne jumamosi ya tarehe 27 mwezi February mwaka huu.

Katika uchaguzo huo Theresia Mbando aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo, aliwataka wajumbe wote kuingia ukimbini ili mkutano huo kuanza.

Baada ya wajumbe kuingia ndani, Mbando alifuata taratibu zote za kiitifaki katika kufungua kikao hicho ikiwa ni pamoja na kugawa ratiba za mkutano huo.

Wajumbe wakiwa tayari kwenda na ratiba ya mkutano huo, ndipo Bi.Sara Yohana (Kaimu Mkurugenzi wa jiji) alisimama ghafla na kutangaza kuhairishwa kikao hicho kwa madai kwamba, amepokea zuio kutoka Mahakama ya Kisutu iliyomtaka kutoendesha uchaguzi huo. Hali hiyo ilizua taharuki na kusababisha vurugu kubwa.


Katika maelezo yake kwa wajumbe Bi.Sarah alionesha nakala ya zuio la Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu iliyotolewa tarehe 5 mwezi February mwaka huu.


Watu wanahoji ikiwa kulikua na zuio la Mahakama kuanzia tarehe 5, kwanini Mkurugenzi aliitisha uchaguzi na kualika wajumbe? Kulikua na haja gani ya kujulisha umma kuwa uchaguzi upo na watu wakafika kumbe kuna zuio la mahakama?

CCM WANA HOFU GANI?
Kutokana na hali inayoendelea yapo maswali mengi yanayoibuka juu ya hofu ya CCM kwenye uchaguzi huu. Je kwanini CCM hawataki kuachia Halmashauri ya jiji iongozwe na upinzani? Wanahofia nini?

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema CCM wana hofu mbili. Kwanza wanahofia kupoteza mamlaka ya kimaamuzi katika mambo yanayohusu maendeleo ya jiji la Dar.

Kwa kuwa jiji litaongozwa na upinzani, CCM watakosa nguvu ya kufanya maamuzi katika mipango ya maendeleo ya jiji, na hivyo watashindwa kutekeleza ilani yao. Hali hii itatoa fursa kwa vyama vya UKAWA kutumia nafasi hii kujiimarisha zaidi kimipango, mikakati na kuwa na mamlaka kuzidi CCM.

Ikumbukwe halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ndiyo inayoongoza kwa makusanyo ya mapato kulinganisha na Halmashauri nyingine nchini. Halmashauri ya jiji la Dar inakadiriwa kukusanya jumla ya shilingi Bilioni 10.7 kwa mwezi, ambapo kati ya hizo Bil 6.9 ni mapato ya ndani na Bil 3.8 ni ruzuku ya serilali. Mapato haya ni makubwa kuliko maapato ya majiji yote yaliyosalia ukiyaweka kwa pamoja.

Pengine hii ndiyo hofu ya CCM. Kwamba wanahofia fedha hizi zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo chini ya utawala wa vyama vya upinzani na hivyo vyama hivi vitapata fursa ya kujiimarisha zaidi.

Lakini upo mtizamo mwingine kwamba hofu ya CCM sio juu ya yatakayofanyika bali juu ya yaliyofanyika. Hawahofii UKAWA watafanya nini wakiingia madarakani, wanahofia wao walifanya nini walipokua madarakani.


Kuna taarifa kuwa kuna uchafu mwingi katika Halmashauri ya jiji la Dar na CCM wanahofia UKAWA wakishinda uchaguzi wataweka wazi uchafu huo.

Yapo madai kuwa miradi mingi ya maendeleo ilitekelezwa chini ya kiwango kwa kuwa wakandarasi walilipwa pesa kidogo kulinganisha na bajeti iliyotengwa. Pesa nyingine zilifanyiwa ufujaji na watendaji wa halmashauri. Hivyo CCM wanahofia ikiwa UKAWA wataingia madarakani watawaumbua.

Mojawapo ya miradi yenue malalamiko mengi ni uuzwaji wa Shirika la la Usafiri Dar es Salaam (UDA) amabalo liliuzwa katika mazingira ya kutatanisha kwa kampuni ya Simon Group ya jijini Mwanza.


Tarehe Mei 24, 2011 Mkurugenzi mkuu wa Simon Group Ndugu Simon Kisena alimuandikia barua Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu akimjulisha kuwa hadi wakati huo yeye ndiye aliyekuwa mmiliki mkuu wa UDA, baada ya kununua hisa 7,880,303 sawa na asilimia 52.35 ya hisa zote za UDA kati ya hisa 15,000,000 za awali kwa gharama ya Sh milioni 285.

Lakini gazeti la Jamhuri la tarehe 26 January mwaka 2016 liliandika habari juu ya ukaguzi uliofanywa kwenye kampuni hiyo ya Simon group na kampuni ya ukaguzi ya Philip & Company ilionesha kuwa Kampuni ya Simon Group ilipata faida ya Bilioni 1.7 baada ya kufanya kazi mwezi mmoja tu tangu walipoinunua UDA.

Yani walinunua UDA kwa Milioni 285 lakini baada ya kufanya kazi kwa mwezi mmoja tu wakapata faida ya Bilioni 1.7. Hii ni faida kubwa sana na isiyotarajiwa katika mazingira ya kawaida.

Ikiwa UDA ilikua na uwezo wa kuingiza faida ya Bilioni 1.7 kwa mwezi kwanini iliuzwa kwa Milioni 285 tu? Bila shaka kuna mazingira ya ufisadi katika sakata la uuzwaji wa UDA. Wapo viongozi kadhaa ambao wamewahi kutuhumiwa kuwa walishiriki kuuza UDA kinyemela.

Huu ni mfano mmoja tu kati ya mifano mingi inayohusu uchafu uliofanyika katika halmashauri ya jiji la Dar wakati jiji likiongozwa na CCM. Na pengine uchafu wa aina hii ndio unaowapa hofu CCM kuachia halmashauri hii kuongozwa na vyama vya upinzani kwa vile wataumbuka.

Kama wameweza kuumbuka Ilala sembuse halmashauri ya jiji? Taarifa ya Meya wa Ilala Mhe.Charless Kwiyeko aliyoitoa mwishoni mwa wiki iliyopita inaonesha kuwa kuna ubadhirifu mkubwa ulifanyika katika halmashauri hiyo wakati ikiwa inaongozwa na CCM.

Mojawapo ni mishahara kwa mgambo wa jiji. Taarifa ya ukaguzi ilionesha kuwa Askari Mgambo wa jiji hulipwa kiasi cha shilingi 280,000/= kwa mwezi lakini malipo halisi waliyokua wakipata ni shilingi 60,000/= kwa mwezi.

Hii ina maana kwamba kila Askari Mgambo alikua akikatwa shilingi 220,0000/= katika mshahara wake ambapo alikua hajui zinapoenda. Huu ni ufisadi na unyonyaji wa kiwango kisichovumilika.

CCM WANA MPANGO GANI?
Hadi sasa CCM wametumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wanaongoza halmashauri ya jiji la Dar lakini imeshindikana. Pamoja na kutumia madiwani kutoka Zanzibar na kuweka zuio mahakamani bado wana hofu ya kushindwa uchaguzi kwa kuwa wana idadi ndogo ya madiwani kulingamisha na wale wa UKAWA. CCM ina jumla ya madiwani 76 na UKAWA 87 hivyo inatarajiwa Uchaguzi ikifanyika CCM wataanguka.

Lakini pamoja na kuwa na idadi ndogo ya madiwani bado wana mpango wa kuongoza halmashauri ya jiji la Dar kwa kutumia mbinu yoyote. Kwa kuwa demokrasia inaonekana kushindwa kuwapa fursa ya kuongoza wanaweza kutumia mbinu nyingine zisizo za kidemokrasia.

Mbinu kubwa inayotarajiwa ni kama ile iliyotumika mwaka 1996. Tarehe 28 mwezi June mwaka 1996 aliyekuwa Waziri Mkuu Mhe.Fredrick Sumaye aliivunja Halmashauri ya jiji la Dar na kuunda Tume maalumu ya muda kwa ajili ya kuongoza jiji hilo kwa madai ya rushwa na jiji kukusanya mapato chini ya kiwango.

Sheria ya serikali za mitaa ya mwaka 1982 [Local Government Act (Urban Authorities) of 1982] pamoja na sheria nyinginezo zinazosimamia serikali za mitaa na majiji zinampa Waziri Mkuu mamlaka ya kuvunja halmashauri ya jiji/mji/manispaa na kuteua Tume ya muda ya kuongoza eneo hilo.

Lakini ili kufanya hivyo ni lazima kuwepo na sababu ya kumfanya Waziri Mkuu kufanya maamuzi hayo. Mwaka 1996 Sumaye aliivunja halmashauri ya jiji kwa kuwa alikua na sababu. Hakuivunja tu kienyeji. Na sabu zenyewe ni mbili. Moja ni madai ya rushwa na pili ni kukusanya mapato chini ya kiwango.

Lakini mwaka huu Waziri Mkuu hana sababu ya kumfanya aamue hivyo. Kama ni mapato, jiji la Dar wanakusanya zaidi ya matarajio. Mwaka 2014/15 walipanga kukusanya Bilioni 10.1 kwa mwaka lakini wakakusanya wastani wa Bilioni 10.7 (zidio la milioni 600).

Kwa hiyo Waziri Mkuu hana sababu ya kuivunja Halmashauri ya jiji lakini CCM wanataka kumpa sababu.

Kitendo cha kuitisha uchaguzi huku wakijua wazi kwamba kuna zuio la Mahakama inaonekana ni mpango wa kuwakasirisha wafuasi wa UKAWA waliokua wamefurika ukumbini ili wafanye fujo na Waziri mkuu atumie fujo hizo kama kigezo cha kuvunja halmashauri ya jiji na kuunda Tume ya muda kuongoza.


Kwa kufanya hivyo atakua amefanikiwa kuhujumu haki ya UKAWA kuongoza jiji la Dar na kuwapa fursa CCM kubaki madarakani kupitia mlango wa uani wa kuunda Tume.

RAIS MAGUFULI ANA NAFASI GANI KATIKA HILI?
Watu wengi wanajiuliza kwanini Rais Magufuli amekaa kimya juu ya suala hili kwa takribani miezi minne sasa. Magufuli ambaye amejitanabaisha kuwa muadilifu kwanini hachukui hatua zozote juu ya swala hili. Kitendo cha kukaa kimya huku akishuhudia demokrasia ikibakwa kinatilia mashaka uadilifu wake.

Hali hii inafanya watu wafike mbali zaidi na kuhoji juu ya ushindi wake. Ikiwa CCM hawako tayari kushindwa katika ngazi ya halmashauri ya jiji, je wangeshindwa katika uchaguzi mkuu nafasi ya Rais wangekubali.?

Ikiwa jambo dogo kama la umeya wamekataa kuheshimu demokrasia, je wanaweza kuheshimu demokrasia katika Uchaguzi ngazi ya kitaifa?

Kwanini Rais Magufuli anatumbua majipu yaliyojificha lakini jipu la Umeya Dar analilea? Kwanini asiwashauri CCM waheshimu demokrasia na maamuzi ya Wananchi?

Miezi minne sasa jiji la Dar es Salaam limesimama. Hakuna mipango ya maendeleo, hakuna vikao vya halmashauri kwa sababu ya CCM kukataa kuheshimu demokrasia. Je Magufuli anaona hili ni sawa?

Kwamba watu waendelee kuteseka kwa kukosa huduma, mipango ya maendeleo isipangwe, kwa sababu tu CCM hawako tayari kushindwa? Je hii ni sawa?

Kitendo cha Rais Magufuli kukaa kimya kwenye suala hili kinamfanya aonekane hana dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko. Hana tofauti na watangulizi wake. Anakipenda zaidi chama chake kuliko anavyowapenda watanzania. Ndio maana yuko tayari kuona chama chake kikivunja demokrasia na wananchi wakiteseka lakini akakaa kimya, kwa sababu tu uvunjaji huo wa demokrasia unakinufaisha chama chake.

Hili ni doa katika utendaji wake, na asipochukua hatua za dharura atapoteza imani yake aliyoanza kuijenga mbele ya jamii ya Watanzania.

Chanzo :Malisa Godlisten

0 comments:

Post a Comment

Top Ad 728x90