Trump alieleza hivi karibuni kuwa atachukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda usalama wa Marekani ikiwa ni pamoja na kuzuia Watu wenye imani ya Kiislamu kuingia nchini humo.
Kauli hiyo ya Trump imeonekana kumkwaza Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ambaye amesema kuwa mtu anayepanga kujenga ukuta kati ya Marekani na Mexico badala ya kujenga daraja ‘sio Mkristo’.
“Mtu anayefikiria kujenga ukuta, kokote walipo, na sio kujenga madaraja, sio mkristo. Hii sio injili,” Papa Francis aliwaambia waandishi wa habari.
Papa Francis alitoa kauli hiyo katika siku yake ya mwisho ya ziara ya Mexico. Alisema kuwa hawalazimishi wakristo kumchagua au kutomchagua mtu fulani, lakini wampime kauli zake kabla ya kufanya maamuzi katika sanduku la kura.
Trump amejibu kauli hiyo ya Papa akieleza kuwa Kiongozi huyo hana haki ya kumhukumu mtu yeyote kuwa ni Mkristo au sio Mkristo.
“Hakuna kiongozi, hususan kiongozi wa dini, mwenye haki ya ya kuhoji imani ya kidini ya mtu mwingine,” Trump alisema.
“Kama Vatican itashambuliwa na ISIS, ambapo kila mmoja anajua kuwa ni tuzo muhimu ya ISIS, ninawaahidi kuwa Papa atatamani na kuomba kuwa Donald Trump angekuwa Rais,” aliongeza Trump.
0 comments:
Post a Comment