Top Ad 728x90

Monday 29 February 2016

Tazama Goli la Kwanza la Samatta Lililoipa Point Tatu Muhimu KRC Genk Dhidi ya Vinara wa Ligi Jana

by
Jumapili ya February 28 Ligi Kuu Ubelgiji iliendelea tena kwa klabu ya KRC Genk inayochezewa na mtanzania Mbwana Samatta kushuka katika uwanja wake wa  nyumbani Cristal Arena kucheza mchezo wake wa 28 wa Ligi Kuu dhidi ya vinara wa Ligi Club Brugge.

Licha ya kuwa Club Brugge walikuwa wanarekodi nzuri dhidi ya Genk wamekubali kipigo cha goli 3-2, kwani kabla ya mchezo huo, Genk na Brugge kwa mechi tano zilizopita, Brugge walikuwa wameifunga Genk mara tatu, sare moja na kupoteza mechi moja

Magoli ya KRC Genk yalifungwa na Nikolaos Karelis dakika ya 31, ikiwa ni dakika 21 zimepita toka Club Brugge wapate goli la kuongoza dakika ya 15 kupitia kwa Thomas Meunier, lakini kasi ya Genk iliongezeka na kupata goli la pili dakika ya 50 kupitia kwa Thomas Buffel.

Mbwana Samatta aliingia dakika ya 79 kuchukua nafasi ya Nikolaos Karelis aliyefunga goli la kwanza la KRC Genk. mabadiliko ya kuingia Mbwana Samatta yalikuwa na faida kwani, dakika 2 baada ya kuingia alipachika goli lake la kwanza akiwa na Genk lakini pia ni goli la tatu kwa Genk, kabla ya dakika ya 83 Brugge walifanikiwa kupata goli la pili.

Mbowe Apinga Watumishi wa Umma Kutumbuliwa MAJIPU Bila Kupewa Nafasi ya Kusikilizwa Kwanza

by
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amepingana  na  sera  ya  Rais John Magufuli  ya kuwatumbua majipu watumishi wa umma wazembe na wabadhilifu wa mali za umma.

Mbowe amedai kuwa Serikali Magufuli imekuwa ikiwatimua watumishi mbalimbali wa umma bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kupitia kampeni ya kupambana na ufisadi, inayotambulishwa kwa kaulimbiu ya ‘utumbuaji majipu’.

Akizungumza jana katika ibada maalumu ya shukrani kwa kumaliza uchaguzi mkuu salama, iliyofanyika kwenye Usharika wa Nshara wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT na kuhudhuriwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Frederick Shoo, na maaskofu wastaafu Dk. Erasto Kweka na Dk. Martin Shao, Mbowe alisema (wapinzani) hawaridhishwi na hatua ya serikali ya Rais Magufuli kuendeleza timuatimua na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma 160 tangu aingie madarakani bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema wapinzani wako tayari kuipongeza serikali wakati wowote inapofanya mambo mazuri kwa manufaa ya taifa, lakini kwa sharti kwamba mara zote iwe inahakikisha sheria za nchi zinasimamiwa, mali na rasilimali za umma zinalindwa na kila kitu kinafanyika kwa kuzingatia taratibu zilizopo.

"Kutokana na hali ya sintofahamu kutamalaki katika taifa kwa sasa, hakuna mtumishi wa umma aliye na amani kutokana na mfumo unaoitwa kutumbua majipu. Tunasikia watumishi wa umma wakifukuzwa kazi bila kusikilizwa.

“Mpaka sasa kuna watumishi 160 wamefukuzwa na wengine kusimmishwa. Lakini pia zaidi ya taasisi na idara za serikali zipatazo 20 hazina uongozi…hii si sahihi,” alisema.

Katika ibada hiyo, Mbowe alikuwa ameongozana na wabunge 16 na makada wengine mbalimbali wa Chadema, alitoa sadaka ya Sh. milioni 279 kwa ajili ya kusaidia ukarabati na upanuzi wa jengo la Bethel lililoko Hai.

"Sisi tunamshukuru Mungu leo kwa kuwa tuko salama ndiyo maana tunatoa sadaka. Sadaka yetu tunaielekeza kwenye upanuzi na ukarabati wa jengo hili la Betheli la Usharika wa Nshara. Kwa hiyo, nawaomba sana viongozi wa dini na Watanzania kuliombea taifa kutokana na hali inayoendelea," alisema Mbowe.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema wabunge 42 wa Chadema wamemuunga mkono kwa kuchangia kanisa hilo Sh. milioni 131.5; mwanasiasa mkongwe na mfanyabiashara, Philemon Ndesamburo alimchangia Sh. milioni 50; marafiki zake wa Arusha Sh. milioni 49.9; Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Edwin Mtei Sh. milioni mbili; makada wengine wa Chadema Sh. milioni 15 na Kamati ya Maandalizi Sh. milioni 41.

Katika hatua nyingine, Mbowe alitumia nafasi hiyo pia kuzungumzia mgogoro wa uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuitupia lawama CCM kwa madai kuwa ndio wanaokwamisha kwa maslahi yao.

Alisema jambo hilo pia linasikitisha kwa sababu sasa ni miezi minne imepita huku haki ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuwa na Meya wao ikiendelea kuminywa kutokana na CCM kutoheshimu demokrasia na kutaka waendelee kuongoza licha ya wananchi kufanya uamuzi wao kupitia sanduku la kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Chadema na Chama cha Wananchi (CUF) vinavyoshirikiana kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ndivyo vyenye idadi kubwa ya madiwani kulinganisha na CCM, hivyo kwa mujibu wa Mbowe, CCM wamebaini kuwa hawawezi kushinda na sasa wanajitahidi kadri wawezavyo kukwamisha uchaguzi huo.

Polisi Yavamia Harusi, Wakamata Bwana Harusi na Watu Wake Kwa Kuhusishwa na Kesi ya Ujambazi Access Bank

by
Baada ya kupitapita huku na kule katika maeneo yaliyotokea kadhia ya ujambazi jana nilifanikisha kunasa tukio Moja maeneo ya Chulwi Kongowe Mbagala kama sijakosea.

Mnamo 27.2.2016 majira ya SAA 12 jioni polisi walivamia harusi iliyokuwa ikifungwa msikitini na kuwakamata watu waliokuwemo ndani wakiwatuhumu kuhusika na Ujambazi uliofanywa siku ya tarehe 26.2.2016 katika tawi moja la Bank ya Access lililoko Mbagala.

Raia walisema polisi ilivamia msikiti na kuwakamata walimu wa dini waliokuwa wakifungisha ndoa hiyo na kuwachukua na kwenda nao hadi ilipo harusi na kuwakamata wengine huku wakiwapiga na kuwatuhumu kuwa wamehusika na ujambazi.

Hata hivyo polisi ilimwachia huru bibi harusi na kuondoka na babu harusi na wapambe wake sehemu kusiko julikana.

Miongoni mwa watu waliokamatwa ni Abdullah Saudi, Juma selemani, Saidi Ally na kassimu Othuman wote wakiwa wakazi wa Mbagala waliokuja kusheherekea harusi ya rafiki yao.

Chanzo: Jamii Forums

Sunday 28 February 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Akagua Bandari ya Mtwara na Kunusa Harufu ya Ufisadi katika Ujenzi wa Gati 3

by
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua bandari ya Mtwara na kunusa harufu ya ufisadi katika utoaji wa zabuni ya ujenzi wa gati mpya tatu.

Waziri Mkuu ambaye alikagua eneo la ujenzi wa gati hizo jana (Jumamosi, Februari 27, 2016), alisema anazo taarifa juu ya utolewaji wa zabuni hiyo na mzabuni ameshashinda lakini kuna madai kwamba watu wa manunuzi kupitia PPRA ndiyo wanakwamisha zabuni hiyo.

Aliwaomba wabunge wa mkoa wa Mtwara washirikiane kusimamia suala hilo ili ujenzi wake uweze kuanza mara moja na kuleta ajira kwa wana Mtwara. "Ujenzi ukikamilika siyo tu ajira zitaongezeka bali hata meli nyingi zitaleta mizigo katika bandari hii na mapato ya mkoa yataongezeka", alisema.

"Natambua kwamba kuna mpango wa kujenga gati nne ambapo moja kati ya hizo itajengwa na TPA (Mamlaka ya Bandari) lakini hizi tatu zilitangazwa na kupata mzabuni ambaye ni kampuni ya Hyundai kutoka Japan. Lakini hii kampuni imekuwa ikizungushwa bila sababu. Tutafuatilia kubaini tatizo liko wapi," aliongeza.

"Sasa hivi tuna uwezo wa kupaki meli moja tu, lakini gati zikikamilika tutaweza kuwa na meli tatu kwa mpigo, cha msingi tusimamie maamuzi yetu kwamba lazima wafanyabiashara wa korosho watumie bandari hii kusafirisha mizigo yao na si kuipeleka kwingine."

 "Kwenye Bodi ya Korosho nako kuna majipu yanahitaji kutumbuliwa. RCC ilishakaa na kupitisha uamuzi kuwa mizigo yote ipitie bandari ya Mtwara lakini kuna watu ndani ya Bosi hiyo wanatoa vibali vya kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam."

Alimtaka mkuu wa bandari ya Mtwara (Port Master) Bw. Prosper Kimaro awe makini na watu wa kitengo cha manunuzi katika bandari hiyo kwani kimekuwa chanzo cha upotevu wa fedha za Serikali kutokana na ujanja wa watu wachache.

"Hapa si kuna mtu alitaka kuiba sh. milioni 300 kwa kufoji saini za wakubwa wake? alihoji Waziri Mkuu swali ambalo lilijibiwa na Bw. Kimaro kwamba ni kweli lakini uongozi uliingilia kati kabla wizi huo haujakamilishwa.

Kuhusu fidia kwa wakazi wa vijiji vya Kisiwa na Mgao ambao wamekubali kuhama ili kupisha upanuzi wa bandari hiyo, Waziri Mkuu aliwahakikishia wabunge hao pamoja na uongozi wa bandari kwamba kiasi cha sh. bilioni 13.8/- kimekwishatengwa na Wizara na kitatolewa mapema mwezi ujao.

Alitumia fursa hiyo kusisitiza udhibiti wa bandari bubu ambazo zinatumiwa kuingiza sukari na mchele mchezo ambao unaikosesha Serikali mapato.

"Mkuu wa Mkoa, nilikwishatoa agizo kama hilo wakati nimeenda kukagua bandari ya Tanga. Kaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nanyi pia muweke mbinu za kudhibiti upenyo huu wa kuingiza bidhaa za magendo kwa sababu hawa ndiyo wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali," alisisitiza.

Mkuu wa bandari hiyo, Bw. Kimaro wakati akitoa taarifa ya utendaji wa bandari mbele ya Waziri Mkuu, alisema bandari hiyo ilianzishwa mwaka 1950 na imekuwa inakabiliwa na ufinyu wa gati ya kuegesha meli, vifaa vya kupakulia na kupakia mizigo na kwamba hivi sasa wamekwishapata winchi ya bandarini (harbour crane) yenye uwezo wa kubeba tani 100 na tayari wako kwenye mpango wa kujenga gati moja.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, FEBRUARI 28, 2016.

Siri ya Matukio ya Ujambazi Dar es Salaam Yawekwa Bayana

by
Wadau mbalimbali wakiwamo wananchi, polisi, Jeshi la Wananchi (JWTZ), Wizara ya Mambo ya Ndani wamezungumzia kuongezeka kwa ujambazi katika jiji la Dar es Salaam.

Baadhi wamesema matukio hayo ya ujambazi yamesababishwa na udhaifu wa Jeshi la Polisi katika kukabiliana na wahalifu wanaotumia silaha kupora fedha kwenye mabenki na maduka makubwa.

Sababu nyingine zinazotajwa ni majambazi hao kuhukumiwa vifungo vya muda mfupi na kutoka gerezani mapema, hali inayorudisha nyuma juhudi za Serikali kupambana na uhalifu.

Kadhalika, umbali wa kituo kimoja cha polisi mpaka kingine, na mara nyingine baadhi kufungwa siku za mwisho wa juma, ni moja ya mambo yanayosababisha kuongezeka kwa uhalifu.

Chanzo kingine kilichotajwa kuchochea ongezeko la uhalifu ni kuhujumiwa kwa Jeshi la Polisi na baadhi ya askari wake ambao ama hutoa silaha kwa wahalifu au kushiriki.

Maoni ya wananchi

Mkazi wa Tandika, Iddi Shomvi alidai jana kuwa majambazi wengi wanaopora fedha kwenye mabenki ni askari wa JWTZ), waliopitia mafunzo ya mgambo, pamoja na polisi. Alisema watu hao ndiyo wenye ujuzi wa kutumia silaha na wanajua zinakopatikana.

“Mwananchi wa kawaida hawezi kutumia silaha za moto wala mabomu. Wanajeshi na polisi ndiyo wanaojua kutumia na wanazo hizo silaha. Nina uhakika kwamba wao ndiyo wanaotupa shida mitaani kwa sababu ya tamaa zao za fedha,” alisema Shomvi.

Alisema ni muhimu Jeshi la Polisi likashirikiana na wananchi kuanzia ngazi za chini ili kuwatambua majambazi na wageni wote walioingia nchini kinyume cha sheria. Alisema baadhi ya wageni nao pia ni chanzo cha kuingia kwa silaha kali nchini.

“Serikali irudishe mfumo wa nyumba kumi ili kila mtu atambulike anafanya nini. Mgeni akija kutoka Burundi, anaweza kuishi na Watanzania bila kufahamika yeye ni nani na anatoka wapi,” alisema.

Mkazi wa Tabata, Severin Lawrence alisema ujambazi unaongezeka kwa sababu utendaji wa polisi ni dhaifu. Alisema inashangaza kuona vituo vinafungwa siku za wikiendi wakati ndiyo zenye matukio mengi.

“Ni jambo la aibu kabisa. Unaona kituo kile cha polisi! Leo kimefungwa. Sasa likitokea tukio la ujambazi hapa tutakimbilia wapi kutoa taarifa?” alihoji kijana huyo huku akionyesha Kituo cha Polisi cha Tabata Relini ambacho kilikuwa kimefungwa.

Lawrence aliitaka Serikali kufunga mfumo wa GPS kwenye pikipiki zote kwa sababu vyombo hivyo vya usafiri ndivyo vimekuwa vikitumika kwenye matukio ya ujambazi. Alisema hilo litasaidia kuwabaini watu wanaojihusisha na ujambazi popote.

Mkazi wa Kitunda, Jumaa Lukindo alisema kitendo cha askari kukaa vituoni kwa muda mrefu kumewafanya wazoeane na wahalifu, jambo linalofanya vita dhidi ya ujambazi jijini kuwa ngumu.

Lukindo alitaka polisi wapewe silaha nzito ili waweze kukabiliana na majambazi ambao nao wanatumia silaha kali.

“Kwenye tukio la ujambazi pale Mbagala, tumesikia kwamba majambazi walitumia pia mabomu ya kutupa kwa mkono. Hao si raia wa kawaida, ni watu wenye ujuzi na mambo ya silaha. Polisi nao wajipange kikamilifu,” alisema.

JWTZ wazungumza

Akizungumzia kuhusika kwa wanajeshi kwenye matukio ya ujambazi, msemaji wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema hakuna uthibitisho wowote kwamba wanajeshi walihusika katika matukio ya ujambazi, hususan lile la Mbagala.

Lubinga alisema mahakama ndiyo inayoweza kuthibitisha baada ya watuhumiwa kukamatwa na kesi zao kusikilizwa. “Siwezi kusema nani anaiba, lakini Tanzania kuna ujambazi. Jambazi anaweza kuwa mtu yeyote, anaweza kuwa padri, sheikh au mwananchi wa kawaida. Lakini hatuwezi kumwita jambazi mpaka itakapothibitika,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje, Charles Kitwanga kuomba msaada ya JWTZ kusaidia vita dhidi ya ujambazi, Lubinga alisema hawajapokea rasmi maombi hayo, lakini watakuwa tayari endapo Serikali itaamua kulitumia katika vita hiyo.

“Serikali ikiamua kuunganisha nguvu, tutakuwa tayari lakini siwezi kusema lini tutaanza operesheni hiyo kwa sababu lazima atangaze Amiri Jeshi Mkuu. Cha msingi majambazi waache kuiba kwa sababu Serikali imechukia na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Kanali Lubinga.

Makamanda wa polisi, Dar

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya alisema kuongezeka kwa matukio ya ujambazi Dar es Salaam kunasababishwa na mambo mbalimbali, kama watuhumiwa kuachiwa huru na mahakama mara wanapokamatwa.

Mkondya alitaja sababu nyingine kuwa ni majambazi wanaokutwa na hatia kufungwa kwa muda mfupi, hali inayosababisha kuendelea na ujambazi mara wanaporudi mtaani na kufanya kasi ya ujambazi kuongezeka.

“Tunaomba Mahakama itusaidie, majambazi hawa wakae magerezani kwa muda mrefu ili wasilete shida mitaani. Sisi polisi pia tutajitahidi kujenga ushahidi mzuri ili majambazi wasiachiwe huru wakifikishwa mahakamani,” alisema.

Kamanda huyo aliwataka wananchi kutoa taarifa polisi kila wanapowaona au kuwahisi majambazi ili nyendo zao zifuatiliwe. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Andrew Satta alisema hawezi kuzungumzia matukio ya ujambazi kwa sababu za kiintelijensia na kuwa upelelezi wa matukio mbalimbali bado unaendelea.

“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio la juzi Mbagala,” alisema kamanda huyo na kusisitiza kuwa wananchi wawe watulivu, polisi wanafanya kazi yao.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, mkuu mpya wa upelelezi wa Kanda ya Dar es Salaam, Camilius Wambura alisema: “Ndiyo kwanza nimeteuliwa, hata sijaripoti kazini. Nikiripoti, nitayasoma na kuangalia namna gani tutayafanyia kazi.”

Mambo ya Ndani

Katibu  Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira alisema anafahamu kuwa matukio hayo ni makubwa lakini hawezi kusema chochote hadi apate ripoti kamili.

Al Shabab Yawaua Watu 24 Kwa Bomu Wakitazama Mechi ya Man U na Arsenal

by
WATU 24 wameuawa na wengine kujeruhiwa kwenye mgahawa mmoja mjini Baidoa, Kusini mwa Somalia wakati wakitazama mechi ya soka baina ya Manchester United na Arsenal baada ya shambulizi lililotekelezwa na Al-Shabab jana jioni.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa milipuko miwili mikubwa ilitokea, katika mgahawa huo uliokuwa umejaa mashabiki wa mechi kati ya Manchester United na Arsenal.

Miongoni mwa wale waliouawa ni pamoja na afisa wa serikali ya jiji hilo.
Mji wa Baidoa ulitekwa na wapiganaji wa Kiislamu wa Al-Shabaab mwaka wa 2008, lakini walitimuliwa mwaka 2012.

Mji huo ulioko takriban kilomita 200 kutoka mji mkuu Mogadishu ni mji wa hivi punde zaidi kushambuliwa na wanamgambo hao wa kiislamu.

Shambulizi la kwanza lilitokea katika mgahawa maarufu unaopendwa na wageni na viongozi wa kisiasa ambao ulishambuliwa kwa gari lililokuwa limetegwa bomu.

Walionusurika waliokolewa na wanajeshi wa muungano wa Afrika AMISOM.
Shambulizi hili limetokea muda mchache tu baada ya kukamilika kwa warsha ya viongozi wa mataifa yanayochangia wanajeshi wake katika jeshi la muungano wa Afrika AMISOM.

Siku ya Ijumaa watu wengine zaidi ya 20 waliuawa katika mgahawa mwengine kufuatia shambulizi la Al Shabaab.

Hii ndio Hofu Kuu ya CCM Kwenye Uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es salaam....

by

Ni wazi kuwa kila jicho la muumini wa demokrasia ,mpenda haki na mpenda maendeleo au mabadiliko limeelekezwa kwenye uchaguzi wa Meya wa Jiji hili linalosemekana kuwa ni jiji la maraha.....ukizingatia kuwa wapinzani (UKAWA) wana uhakika wa kumtoa meya kwa asilimia zaidi ya mia kutokana na wingi wa wapiga kura kwenye uchaguzi huo hivyo kuongeza msisimko zaidi kwenye uchaguzi huo....

Sarakasi zinazofanywa na serikali ya CCM kupitia mamlaka yao katika kuukwamisha uchaguzi huo zinazusha maswali mengi katika vichwa vya wapenda haki na waumini wa mabadiliko.....
Kiukweli ni miujiza pekee ndiyo itakayofanya CCM kuchukua kiti cha umeya mwaka huu kwa kutazama tu idadi ya wapiga kura(madiwani)..labda na ubabe ambao wameshauzoea kuufanya.....

Sasa swali la msingi ni kwamba ni kwanini hasa serikali ya CCM inaogopa jiji la Dar es salaam lote kuwa chini ya UKAWA....???

Jibu lake ni kwamba serikali ya CCM inaogopa kuwa UKAWA watakapochukua mamlaka za jiji lote la Dar es salaam ule Wizi wao, uchafu wao,Ufisadi wao na ukiritimba wao utakuwa bayana machoni mwa wananchi hivyo kuzidi kuwapa wakati mgumu zaidi katika nyakati zijazo za chaguzi mbali mbali hasa ikizingatia kuwa wananchi wa nyakati hizi kidogo wana uelewa wa mambo na uthubutu wa kuhoji mambo mbali mbali yanayo wagusa moja kwa moja....


Ni kichaa pekee ndiye asiyejua kuwa jiji la Dar es salaam ndio jiji linaloongoza kwa kukusanya mapato mengi zaidi kutokana na wingi wa watu na biashara mbali mbali zinazofanyika ndani ya jiji hili....lakini mapato hayo yanakutana na mchwa wengi wenye meno makali ya kutafuna visivyo halali yao.....hivyo kufanya hali ya mandhari ya jiji kutoendana na makusanyo yake...

Kutokana ufisadi na wizi wa mapato katika jiji hili imefanya jiji hili kuongoza kwa uchafu kila mahali hadi katikati ya jiji.....imefanya jiji hili kuwa na hali mbaya kiusalama hasa nyakati za usiku kutokana na kutokuwa na mataa ya mitaani...mabara bara mengi ya jiji hili hayapitiki hasa kipindi cha mvua kutokana na ubovu wake na miundombinu chakavu ya mifumo ya maji taka....yapo mambo mengi mabaya ambayo nikiyaa orodhesha hapa inaweza kuchukua hata masaa mawili...lakini mambo yote hayo hayaonekani na viongozi wa manispaa mbali mbali za jiji hili kwa kuwa vipaumbele vyao ni kuyatumikia matumbo yao na sio wananchi........

Habari njema ni kwamba UKAWA kupitia mipango na mikakati yao mizuri wanataka kuibadilisha hali hii ndani ya jiji hili....wanataka kuifanya Dar es salaam iwe na hadhi sawa na majiji mengine huko duniani....wanataka kuiweka Dar es salaam katika sura nyingine kabjsa.....wanataka Dar es salaam ipige hatua kutoka hapa ilipo jambo ambalo serikali ya CCM ililishindwa kwa kipindi chote cha uongozi wao...

Ninachowaomba wanaCCM ni kwamba lazima wajue kuwa nyakati zinabadilika hivyo wanatakiwa waendane na wakati...kama tuliwapa mamlaka kwa kipindi chote hicho na wakashindwa kutuondolea kero za jiji na ndio sie tulioamua kuwapumzisha kupitia masanduku ya kura tukitaka tuangalie pia uwezo wa wengine katika kutatua kero za jiji hili....hata wao wasipoturidhisha tutawapumzisha.....
Waache demokrasia ichukue mkondo wake....

Nawasilisha......

Chanzo:KikulachoChako

Baada ya Majambazi Kuvamia Benki ya Access Tawi la Mbagala....Polisi Waomba JWTZ Kusaidia Vita Dhidi ya Majambazi

by

Siku moja baada ya majambazi kuvamia Benki ya Access Tawi la Mbagala Rangi Tatu, kuua watu watatu akiwamo Polisi na kujeruhi watu wengine watatu akiwamo polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga amesema wataomba msaada wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ili kukabiliana na matukio ya ujambazi.



Alisema Jeshi la Polisi linajipanga upya kuhakikisha wananchi wanakuwa na amani kwa kuwashughulikia majambazi popote walipo.




Waziri Kitwanga alisema wanaanza na Mkoa wa Pwani, kwa kuhakikisha wanawasaka na kufyeka mapori yote ya Bagamoyo na kwingineko ili kuvunja mtandao wao.




“Kama walidhani Jeshi la Polisi limelala lipo macho, walichofanya ni kama wamemuamsha aliyelala, tutawasaka, tutawakamata na tutawapeleka kwenye mkono wa sheria na tutahakikisha tunawamaliza wote,” alisema Kitwanga.




Alisisitiza kuwa wanaotumia pikipiki nguvu ya ukaguzi itaongezwa dhidi ya vyombo hivyo, kwa sababu inaonekana wahalifu wengi hasa majambazi hutumia usafiri huo kutekeleza uovu wao.




Akielezea tukio la uporaji wa Mbagala, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema wamefanikiwa kuwaua majambazi watatu kati ya 12 waliofanya uvamizi huo.




Alisema majambazi hao walikufa baada ya kupigwa risasi katika majibizano ya risasi na Polisi katika Kijiji cha Chui Mkuranga, baada ya kujaribu kutoroka walipozidiwa nguvu.




Alisema majambazi hao wakiwa na pikipiki sita, huku kila moja ikiwa na majambazi wawili waliokuwa na bunduki aina ya SMG na mabomu ya kutupa kwa mkono, walivamia benki hiyo na kuwashambulia kwa risasi kisha kuwajeruhi wafanyakazi wa benki hiyo waliokuwa katika chumba cha kuhifadhia fedha.




Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Salum Juma na Francis Amani, na kupora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa kati ya Sh20 na 30 milioni za kaunta baada ya kushindwa kuvunja chumba cha kuhifadhia fedha.




Alisema kabla ya kuingia ndani, walivamia kibanda cha walinzi na kumpiga risasi askari mwenye namba H7739PC Khalid Juma ambaye alifariki dunia papo hapo.




Pia, walimjeruhi kwa kumpiga risasi kwenye nyonga askari Shaban, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili na kupora bunduki mbili.




Kamanda Sirro alisema majambazi hao baada ya kufanya uporaji walipokuwa wanaondoka, walifyatua tena risasi iliyompata kidevuni na kumuua papo hapo Abdi Salum, ambaye ni muuza duka jirani na benki hiyo na Baraka Fredrick, mlinzi wa kampuni ya Security Group of Africa.




“Hata hivyo Polisi wamefanikiwa kukamata bunduki tatu kati ya hizo mbili ni mali ya Polisi, mabomu matatu ya kutupa kwa mkono na pikipiki sita zilizokuwa zikitumiwa na majambazi hao walipozidiwa nguvu walizitelekeza na kukimbia,” alisema Sirro.




Katika hatua nyingine, Februari 18, eneo la Kiwalani polisi walikamata majambazi watatu wakiwa na bastola moja na Februari 24 eneo la Upanga karibu na Daraja la Sarender, askari waliwakamata watuhumiwa watatu kwa makosa ya kujihusisha na ujambazi wa kutumia silaha.




Kamanda Sirro alisema baada ya kuwahoji walikiri kufanya matukio ya ujambazi wa kutumia silaha na kumtaja mtuhumiwa mwenzao mmoja anayeishi Tabata Kinyerezi jijini Dar es Salaam.




“Alipofuatwa nyumbani kwake, alikutwa na sare za jeshi hilo, redio ya upepo na pingu,” alidai kamanda huyo.

Mahakama Yasikitishwa na Hamaki za Steven Wasira Baada ya Kushindwa Kesi na Ester Bulaya Mpaka Kutaka Kumwagushia Mwandishi Kipigo..

by

Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza umeelezea kusikitishwa na kitendo cha Waziri wa zamani wa kilimo, chakula na ushirika, Stephen Wasira kutaka kumshambulia mpigapicha wa gazeti hili, Michael Jamson na kumzuia kutimiza wajibu wake.

Akizungumzia tukio hilo juzi, Naibu Msajili Mwandamizi wa mahakama hiyo, Francis Kabwe alisema ofisi yake imesikitishwa na kitendo hicho kwani ni kuingilia uhuru wa vyombo vya habari katika kutimiza wajibu kwa jamii.

Hata hivyo, alisema mahakama haiwezi kuchukua hatua yoyote dhidi ya Wasira kwa sababu tukio hilo lilitokea nje ya chumba cha mahakama.

“Tukio hilo lingetokea mbele ya mahakama wakati shauri linaendelea ingehesabiwa kuwa ni kuingilia uhuru wa mahakama na makahama ingechukua hatua, lakini kwa sababu lilikuwa nje ya mahakama, mikono yetu imefungwa labda vyombo vingine vinaweza kuingilia,” alifafanua Msajili

Alisema ushahidi wa picha zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari vikimuonyesha Wasira akimkimbiza mpigapicha huyo ulimshtua, hasa ikizingatiwa umri na nyadhifa za kiserikali alizowahi kushika kiongozi huyo aliyedumu kwenye uwaziri tangu Serikali ya awamu ya kwanza.

Katika tukio hilo lililotokea Jumatano iliyopita, Jamson alinusurika kupigwa na Wasira aliyechukizwa na kitendo cha kumpiga picha, akiwa ameambatana na wadai katika shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi jimbo la Bunda. Wadai hao, Magambo Masato na wenzake wanne waliofika mahakamani hapo kusikiliza uamuzi wa mahakama kuhusu ombi la kukata rufaa kupinga shauri lao kutupwa, ambalo pia lilitupwa.

Akizungumza na Mwananchi juzi, Wasira alisema alilazimika kumuandama mpigapicha huyo baada ya kumpiga picha nyingi isivyo kawaida.

"Haiwezekani mtu anakupiga picha mia moja eti zote ni za habari? Najua fitna za uchaguzi bado zinaendelea na inawezekana huyu kijana anatumiwa na wanasiasa,” alisema Wasira

Usione Vyaelea Ujue Vimeundwa....Siri ya Shule 10 Bora Tanzania Matokeo ya Kidato Cha Nne Hadharani

by

“Usione vyaelea vimeundwa”, huo ni msemo wa wahenga ukimaanisha kila mafanikio yana maandalizi.

Msemo huo unaendana na kilichotokea katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne yaliyotangazwa wiki iliyopita, ambapo katika shule 10 zilizofanya vizuri hakuna hata moja yenye maandalizi hafifu. Shule nyingi kati ya hizo ada zake ni kuanzia Sh8 milioni hadi tisa kwa mwaka.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa shule hizo zote ni zenye majengo mazuri, walimu wazuri na wenye motisha, maabara zilizokamilika sehemu nzuri za kulala na zinazotoza ada zaidi ya Sh2.5 milioni, mbali ya gharama nyingine za chakula, malazi na vitabu.

Shule 10 zenye watahiniwa zaidi ya 40 zilizoshika nafasi za kwanza ni Kaizirege ya mkoani Kagera, Alliance Girls ya Mwanza, St. Francis Girls (Mbeya), Alliance Boys ya Mwanza, Canossa (Dar es Salaam), Marian Boys (Pwani), Alliance Rock Army (Mwanza), Feza Girls na Feza Boys (Dar es Salaam) pamoja na Uru Seminary (Kilimanjaro) ambayo ada yake imetajwa kati Sh1.5 milioni au Sh1.6 milioni kwa mwaka .

Uchunguzi huo umebaini shule tano kati ya 10, zilizoongoza ada zake ni kuanzia Sh8 milioni hadi tisa kwa mwaka.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kaizirege iliyoshika nafasi ya kwanza, kila mmoja analipa Sh2.5 milioni za ada. Malipo yote hayo kwa shule zote 10 ni tofauti na gharama za malazi, chakula na vitabu ambavyo malipo yake yanajitegemea.

Kwa makadirio ya ada pekee, mwanafunzi atakayesoma shule hii kwa miaka minne endapo ada hiyo haitaongezeka, atapata elimu hiyo bora katika mazingira mazuri ya kufundishia, lakini lazima awe na Sh10 milioni.

Meneja wa shule hiyo, Eulogius Katiti alisema wanafunzi wanasoma katika mazingira bora, sehemu nzuri ya kulala, chakula bora, vifaa vyote vya kufundishia na hakuna somo linalosomwa kwa nadharia, yote husomwa kwa vitendo kama inahitajika kufanya hivyo.

“Angalia kwenye mtandao, utaona ubora wa mazingira ya shule, mabweni, jumlisha na matokeo ya mwisho ndiyo utaona ni kwa jinsi gani fedha yao inafanya kazi na kuwapa kilicho bora,” alisema Katiti.

Shule ya wasichana ya St. Francis iliyopo mkoani Mbeya, iliyoshika namba tatu, ili mwanafunzi ajiunge na shule hiyo, anatakiwa alipe ada ya Sh2.2 milioni kwa mwaka, huku akitakiwa kulipa katika mikupuo minne.

Mwanafunzi anayesoma katika shule hiyo, anatakiwa kulipa kiasi cha Sh8.8 milioni kwa miaka minne (endapo ada itabaki palepale) mbali ya kulipia bweni, vitabu, chakula na malazi.

Katika Shule ya Sekondari ya wasichana Canossa ya Dar es Salaam, mzazi anahitaji kuwa na Sh3 milioni, ili mwanaye asome mwaka mmoja shuleni hapo, zikiwamo gharama za malazi, chakula, vifaa vya kusomea na ada.

Kwa maana hiyo kwa miaka minne anatakiwa kuwa na kiasi cha Sh12 milioni ili aweze kusoma shule ya Canossa.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Feza Boys ada ni Sh2.9 milioni, lakini ikijumlishwa na gharama za chakula, malazi na vifaa vya masomo, jumla inafika Sh8 milioni na ushehe, ikiwa ni chini kidogo ya Sekondari ya Feza Girls ambazo gharama yake inafikia Sh9 milioni kwa mwaka.

Mkuu wa taaluma wa shule hiyo, Zakia Irembe alitetea gharama hizo, akisema zinaendana na kiwango cha elimu anachopata mwanafunzi na utulivu anaokuwa nao awapo shuleni hapo.

Alisema hakuna kitu kigumu katika masomo kama kusoma huku mwanafunzi anawaza atakula nini, hana uhakika wa kulala, lakini kwao chakula bora, malazi ya kuvutia, uhakika wa kufanya vizuri kutokana na weledi wa walimu katika kufundisha ndiyo siri pekee ya mafanikio yao.

Irembe alisema katika mlo wa wanafunzi kila wakati lazima kuwe na matunda, huku wanafunzi hao wakiwa hawali ugali na kufua nguo ni uamuzi wa mwanafunzi ama atumie mikono au mashine, uhakika wa umeme, kamera za CCTV kwa ajili ya usalama na kila bweni lina eneo la kupumzikia kutizama taarifa ya habari.

“Mzazi analipa fedha anabaki anatudai elimu, jukumu la kusimamia chakula, malazi ni letu, ndiyo maana vitu vyote kwetu ni bora ili kupata elimu bora pia. Elimu inahitaji uwekezaji mkubwa, kusoma siyo kila mtu anaweza, kunahitajika vitu vya ziada kuhakikisha akili ya msomaji inawaza masomo pekee,” alisema Irembe.

Mwanafunzi aliyeshika namba moja katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, Butogwa Shija aliyekuwa akisoma katika Shule ya Wasichana Canossa, alisema kuwa licha ya kupenda kusoma, mazingira mazuri ya kusomea, uhakika wa kupata kila anachotaka katika kujifunza ndiyo chachu ya mafanikio yake.

Mzazi wa mwanafunzi Innocent Lawrence aliyeshika nafasi ya tatu katika mtihani huo kutoka Feza Boys, Lawrence Nyakabunda alisema kuwa ada anayolipa katika shule hiyo inalingana na elimu anayopata mwanaye.

Alisema anakubaliana na ada kuwa kubwa, lakini anaridhishwa na kiwango cha elimu kijana wake anachopata.

Wakati wenye shule na wazazi wakisema hayo, Msomi wa masuala ya elimu, Profesa Kitila Mkumbo alisema sababu kubwa ya shule hizo kufanya vizuri ni aina ya wanafunzi wanaochukua, wanakuwa wamechujwa hadi wanapofika katika mtihani wa mwisho wote wanakuwa bora.

Alisema shule hizo pia zina walimu wa kutosha, wenye weledi wa ufundishaji, huku wakipewa motisha ya kufanya kazi hiyo.

Breaking News:Walimu Wote wa Shule za Sekondari na Msingi Jijini Dar Kuanza Kusafiri Kwa Daladala Bure

by

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda kwa kushirikiana na wamiliki wa vyombo vya usafiri Dar es salaam wametangaza kuanzisha mpango wa kuwasaidia Walimu wa Shule za Serikali kwa kuwapatia huduma za usafiri bure katika daladala.
Akieleza mbele ya waandishi wa habari Makonda amesema ‘Nilianza kuongea na vyama vya usafirishaji kisha kujenga hoja dhidi ya changamoto za Walimu wetu, na nikawaomba viongozi hao tuonane kulijadili hili na kisha tukafika muafaka ’

‘Na muafaka huo ningependa kuwatangazia Walimu na Watanzania, yakwamba sasa kuanzia tarehe 7/3/2016 Walimu wa Shule za msingi na wasekondari watasafiri bure kwenye vyombo vyetu vya usafiri kwa Mkoa wa Dar es salaam’

‘Tumeweka utaratibu, Walimu watalazimika kutengenezewa vitambulisho maalum ambavyo kila Shule itatengeneza vitambulisho vyake, huku kukiwa na mambo manne ya kuzingatia ambayo ni 1. Picha ya Mwalimu husika, 2. Jina la shule 3. Namba ya Mkuu wake wa shule 4. Kuwe na sahihi ya Mkuu wa Wilaya Paul Makonda’

Dudu Baya Awaka Baada ya Kuambiwa ni ‘Baba wa Nyumbani’ Hana Cha Kufanya

by

Mashakibi wa muziki wamemtibua Dudu Baya baada ya kumwambia amekosa cha kufanya ndio maana amekuwa akiwatukana wasanii wenzake ovyo.

Rapa huyo ambaye ameachia wimbo ‘Kokoriko’ hivi karibuni, ameiambia Bongo5 kuwa mashabiki wanashindwa kujua kuna vitu gani nyuma ya pazia ya maisha ya wasanii.

“Kuna mashabiki nimewaona Enewz ya EATV wanasema nimekosa cha kufanya ndio maana nakaa tu nyumbani, nataka wajue muziki sio mkojo ukijisikia tu unautoa mashabiki wajue, mpaka kazi inatoka wajue kuna kazi kubwa imefanyika” alisema Dudu Baya.

Aliongeza,
“Mimi bado ni mfanyabiashara, Je kampuni ya Mambaz Timber ni yao?. Je kampuni ya Mambaz Entertaiment ni yao?. Kama ni mamluki wajipange, mimi ni Mamba na wasione nipo kimya katika muziki wakadhani sina cha kufanya.Kukaa maskani ni sehemu ya maisha yangu na sitaacha na si kila mtu na sio lazima ajue shughuli zangu zingine,”

Madudu 14 Yabainika Vitabu vya Darasa la Kwanza...Watendaji Watatu Wasimamishwa Kazi

by

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imebaini kasoro 14 katika uchapaji wa vitabu 2,807,600 vya darasa la kwanza.

Kutokana na ‘madudu’ hayo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Maimuna Tarishi jana alitangaza kuwasimamisha kazi watendaji watatu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kuhusishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Tarishi alivitaja vitabu hivyo kuwa ni pamoja na cha Najifunza kusoma, kitabu cha kwanza na Najifunza kusoma, kitabu cha pili.

Tarishi alisema kasoro hizo zimesababisha wanafunzi wa darasa la kwanza wa mwaka 2016 kukosa vitabu kwa kuwa haviwezi kutumika.

Waliosimamishwa kazi ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Idara ya Vifaa vya Kielimu, Peter Bandio, Mwanasheria wa taasisi hiyo, Pili Magongo na Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Jackson Mwaigonela.

Kasoro zilizomo

Katika vitabu hivyo imebainika kuna mwingiliano wa rangi, upungufu wa kurasa, picha ya aina moja kuwa na rangi tofauti katika vitabu, ukataji usiozingatia vipimo, baadhi ya vitabu kufungwa kwa pini moja, vingine kukosa pini kabisa na baadhi kufungwa ubavuni.

Kasoro nyingine ni kuchakaa kabla ya matumizi hasa kitabu cha ‘Najifunza kusoma’ kitabu cha pili, mpangilio mbaya wa kurasa, ufifiaji wa maandishi, picha na baadhi ya vitabu maandishi kufutika.

“Tumebaini baadhi ya vitabu kugeuzwa mwelekeo, majalada kuwa zaidi ya moja na baadhi ya vitabu vimerudufiwa ‘fotokopi’,” alisema.

Alipoulizwa ni vitabu gani vitatumika badala yake, Tarishi alisema vitaendelea kutumika vitabu teule vilivyochapishwa na kampuni binafsi pamoja na vile vya Kiongozi cha Mwalimu.

Alisema Kampuni ya Yukos iliyochapisha vitabu hivyo, pia haikuzingatia vigezo vilivyowekwa, kwa maana nyingine imekiuka makubaliano yaliyo katika mkataba iliyoingia na TET.

Tarish aliitka iondoe vitabu vyote ilivyochapisha kwenye ghala la Serikali ifikapo kesho.

Ilivyotokea

Ili kutekeleza mtalaa mpya wa darasa la kwanza na la pili, Aprili 3 mwaka jana, TET ilitangaza zabuni ya kuchapa vitabu vya kiada vya darasa la kwanza, wachapishaji watatu walishinda zabuni hiyo ambao ni Jamana Printers Limited, Tanzania Printing Services na Yukos Enterprises Ltd.

“Kampuni ya Yukos Enterprises Ltd ilishinda zabuni ya kuchapa vitabu hivyo. Ufuatiliaji uliofanywa na wizara katika bohari ambayo ilikuwa ikipokea vitabu hivyo, ulibaini kuwa vitabu vilivyowasilishwa vilikuwa na kasoro 14,” alisema Tarishi.

Alisema Januari 22, mwaka huu, uongozi wa taasisi ya elimu ulishauriwa usitishe uchapaji wa vitabu uliokuwa ukifanywa na Kampuni ya Yukos ili Serikali isiendelee kupokea vitabu vyenye kasoro.

“Hata hivyo TET haikusitisha uchapishaji wa vitabu hivyo na badala yake kampuni hiyo ilichapa vitabu vyote ilivyopangiwa,” alisema.

Hasara iliyopatikana

Tarishi alisema, “Serikali haijaingia hasara yoyote kwa sababu aliyepewa zabuni alilipwa asilimia 20 ya zaidi ya Sh2 bilioni na makubaliano yalikuwa kama akishindwa kutimiza masharti ya mkataba, pesa aliyolipwa atairejesha.”

Mwili wa Marehemu Uliyozikwa Kikristu Wazua Zogo Waislam Waandamana Wakitaka Kuufukua Mwili Uzikwe Kiislam

by


KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida waumini wa dini ya kiislamu pamoja na viongozi wa dini hiyo wilaya na mkoa wa Geita, wameandamana mpaka kwenye familia ya marehemu Samweli Malugala  wakitaka kufukua mwili wake uliozikwa kikristu na ndugu zake.

Sakata hilo limekuja siku moja baada ya kuzikwa nyumbani kwao katika mtaa wa Mkolani kata ya Nyankumbu mjini Geita, ambapo viongozi wa dini ya Kiislamu walifika nyumbani kwa marehemu kutoa zuio la kuzikwa, na kwa vile hawakuwa na vigezo hawakuweza kufanikiwa kusudio lao.

Jana majira ya saa sita mchana Waislamu wakiwa wameongozana na maimamu wa msikiti wa ijumaa mjini Geita pamoja na mwenyekiti wa bakwata Mtaa wa Kalangalala walifika mpaka kwenye familia ya marehemu Samweli na hapa na kuanza kuongea kilichowapeleka.

Naye mwanafamilia Lucas Paul ambaye ni mtemi wa sungusungu Mtaa wa Mkolani , amewataka wafuate taratibu ya kufanya zoezi lao wakiwa chini ya uongozi wa Mtaa au Kata.

Muda mfupi baada ya malumbano hayo, mkuu wa polisi wilaya ya Geita  Ali kitumbo amefika katika enao hilo la tukio  na kuwataka Waislamu wafuate taratibu na kwamba wao polisi  wako tayari kusimamia zoezi hilo.

Pamoja na kwamba marehemu amekwisha zikwa kikristu kesi ya msingi itaanza kusikilzwa tarehe moja mwezi machi mwaka huu katika mahakama ya wilaya ya Geita, ambapo itaamua nani ana uhalali wa kuuzika mwili huo.

Utafiti Waonyesha Wanaume Wenye Vipara Wana Mvuto zaidi Kimapenzi Zaidi ya Wenye Nywele

by


Kuna vitu vingi humvutia mtu inapokuja swala la kumchagua mpenzi, siwezi taja sifa zote, kila mtu anasifa zake na vigezo vyake, ila ngoja tuongelee mvuto wa kipekee unaopatikana kwa wanaume wenye vipara.

Nikiongelea vipara naongelea wale walio na vipara asili, achilia mbali wale wanaopenda kunyoa vipara japokuwa kuna baadhi ya sifa hapa wanaweza wakawa nazo pia.

Muonekano wa kiume: wanaume wenye vipara wengi huwa na muonekana wa kiume zaidi,muonekano nadhifu  sina maana kama wanaume wengine walio na nywele ndefu ama wastani hawana mvuto lah, nauongelea mvuto zaidi ama mvuto wa kipekee.

Ujasiri: wanaume wa aina hii wengi huonekana ni wajasiri kwa muonekano wao tu, hii huwafanya kuwa kivutio kwa wanawake.

Wana hisia kali za kimapenzi: daktari kutoka Chuo cha Yale Marekani , James B. Hamilton alisema katika utafiti wake wanaume wengi walio na vipara miili yao huwa inazalisha mbegu nyingi za kiume kuliko wanaume wenye nywele, japokuwa si kwa asilimia 100 alisema pia  uchunguzi zaidi bado unaendelea ili kutetea uchunguzi huo.

Hawana muda na Vioo: mwanaume anaefuga nywele ndefu hutamani aonekane msafi na mtanashati kwahiyo hatokaa mbali na kitana chake wala mbali na kioo chake, labda tu awe ana Rasta. Mwanaume mwenye vipodozi vingi kwaajiri y aywele zake kumshinda msichana

Wastarabu : kuna utofauti wa muonekano kati ya mwanaume mwenye kiduku, na suti na mwenye upara na suti  watu hawa wawili wanaweza kuonekana tofauti sababu tu ya nywele zao,muonekano wao unaweza ongelewa tofauti mbele za watu.

Wapo tayari kwa mabadiliko:  kama mtu ameweza kukubali kwamba hawezi kuwa na nywele kama watu wengine na akaibubali hali yake, tofauti na wale wanaovaa kofia sana na wengine nchi za nje wanavaa hata mawigi  ili wasionekana hawana nywele. Lakini wapo wanao ichukulia kama hali ya kawaida hawa ni zaidi ya wajasiri. Wanaweza kuvumilia

Vin Diesel, L.L. Cool J, Bruce Willis, Michael Jordan and The Rock (Dwayne jonhnson  hawa ni Baadhi tu ya mastaa  kutoka Marekani. Ambao wana vipara.

Saturday 27 February 2016

Dogo Janja Kumshitaki Msichana Aliyemrekodi Kwenye Mazungumzo yao Wakati Amkimtongoza

by

Msanii wa bongo fleva ambaye ameachia wimbo wake mpya wa My Life,dogo Janja amesema kuwa tayari ameshakuchukua RB polisi kwa ajili ya msichana aliyerekodi mazungumzo yao ya siri na kuyavujisha mtandaoni.

Dogo Janja aliyasema hayo kwenye moja ya mahojiano yake wakati anaachia wimbo wake mpya na kueleza ni jinsi gani msichana huyo alivyompa wakati mgumu.

“baada ya kusikia ile voice note akili yangu ili stuck,zikawa zinaingia simu nyingi hasa za nyumbani wakinilaumu,nikajaribu kumcheki yule msichana akani block mpaka sasa kani block ila nina RB yake” alifunguka dogo janja.

Sijui Kama Wema Sepetu Alishawahi Kuwa na Mimba -Mirror

by

Msanii wa muziki wa bongo fleva Mirror, anayefanya kazi chini ya Wema Sepetu amesema hajui kama Wema alishawahi kuwa na mimba ila na yeye anasikia kwa watu na kwenye mitandao.

Msanii huyo ambaye anatamba na wimbo wake mpya Naogopa ambao ameimba na Baraka Da Prince ameyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano katika kipindi cha ENews kinachorushwa na EATV.
Mirror amesema hafahamu chochote kuhusiana na jambo hilo na wiki 2 zilizopita nilikuwa naye ofisini lakini sikuona kama kuna tatizo lolote yupo ana furaha na anaendelea na kazi zake kama kawaida .

Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Idriss Sultan alinukuliwa akisema watoto wake mapacha ambao walikuwa wapatikane kupitia Wema haikuwa bahati,kuwaona.

CUF Kuandamana Kupinga Marudio Ya Uchaguzi Zanzibar..Wadai Hali ya Zanzibar si Shwari Watu Wanaishi Kwa Hofu..

by

CHAMA cha Wananchi (CUF) Bukoba kimejiandaa kufanya maandamano ya amani keshokutwa, kwa ajili ya kupinga kufanyika upya uchaguzi wa Zanzibar unaotarajiwa kuwa Machi mwaka huu.

Kimeiomba pia serikali ya awamu ya tano, kuchukua uamuzi wa kumtambua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa urais Zanzibar na kuwa hakiko tayari kurudia uchaguzi huo tena.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama hicho, Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho Saverina Mwijage, alisisitiza kuwa kamwe chama hicho hakitakuwa tayari kurudia uchaguzi huo uliotangazwa na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa utafanyika Machi 20,kwa kile kinachodaiwa ni kufutwa uchaguzi wa Oktoba 25,mwaka jana.

“Tumedhamiria kuandamana ili kumfikishia ujumbe wetu Rais John Magufuli kupitia kwa Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongella lengo letu hasa ni kupinga uchaguzi wa Zanzibar. Hali ya Zanzibar kwa sasa haiko shwari, watu wanatishiwa maisha yao, wanaishi kwa hofu juu ya maisha,” alisisitiza.

Mwijage ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF Taifa, alisema chama hicho kinatambua uchaguzi ulishakwisha na tume hiyo ilishatoa vyeti kwa walioshinda, kwa mantiki hiyo CUF inamtambua Maalim Seif kuwa alishinda katika uchaguzi huo.

Alisema maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri na baadaye utakuwepo mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mayunga ulioko mjini Bukoba ili kuutangazia umma juu ya msimamo wa chama hicho na baada ya hapo watazunguka katika wilaya za Muleba, Missenyi na Karagwe.

Majambazi Dar es Salaam Yavamia Benki Ya Access....Yaua Mlinzi na Kupora Pesa, Polisi Wapambana Nayo na Kuyaua

by

Majambazi  ambao  idadi  yao  haikufahamika  wakiwa  na  mabomu  na  bunduki  za  kisasa  jana  walivamia  Benki  ya  Access  tawi  la Mbagala  ambako  walipora  viroba vya   fedha, kuua  mlinzi  na  baadae wanne  kati  yao  waliuawa  na  jeshi  la  polisi.

Watu  walioshuhudia  tukio  hilo  walisema  baada  ya  majambazi  hao  kufika  katika  benki  hiyo  kwa  bodaboda  nne  majira  ya saa  nane  mchana,yalimuua  mlinzi  wa  benki  hiyo, kusha  kubomoa  kwa  risasi  mlango  wa  vioo  na  kuingia  ndani  na  kuzua taharuki  kubwa

Mashuhuda  hao  walisema, katika  tukio  hilo  lililodumu  kwa  karibu saa  moja,mmoja  wa  majambazi  hao  aliyekuwa  amevaa  kininja,alikuwa barabarani  akiamuru  magari  kupita  haraka  huku  akifyatua  risasi  hovyo.

Ilielezwa  kuwa, jambazi  huyo  aliyeonekana  kuwa  na  uzoefu  wa  matumizi  ya  bunduki  alikuwa  akifyatua  risasi  kwa  kutumia  mkono  mmoja  na  ndiye  aliyewajeruhi  baadhi  ya  wapita  njia.

Hivyo,wakati  uporaji  ukiendelea  na  jambazi  huyo  akiimarisha  ulinzi  barabarani  baadae  hakukuwa  na  magari  wala  pikipiki  zilizokuwa  zikipita.

Mfanyabiashara  wa  duka  la  vifaa  vya  ujenzi  jirani  na  benki  hiyo,Ramadhani Tairo  alisema  baada  ya  jambazi  huyo  kuliona  gari  la  polisi  likielekea  eneo  la  tukio,alifyatua  risasi  na kulipiga  kabla  halijafika.Gari  hilo  lilipoteza  mwelekeo  na  kutumbukia  mtaroni.

Tairo  alisema  mbali  na  jambazi  huyo  kulipiga  risasi  gari  la polisi  pia  alilirushia  bomu  la  mkono,lakini  liliangukia  barabarani  bila  kuripuka.Polisi  walifanikiwa  kulilipua  bomu  hilo  baadae  likiwa  halijasababisha  madhara  kwa wananchi  waliofika  kushuhudia  tukio  hilo.

Mkazi  mwingine  wa  eneo  hilo,Rebecca  Maliva  alisema  majambazi  walioingia  ndani  ya  benki  hiyo  walioneka  wakitoka  na  viroba  vitatu vya  fedha  ambavyo  walivipakata kwenye  pikipiki  na  kuondoka  kwa  kasi  kuelekea  Mkuranga kupitia  barabara  ya  Kilwa.

Rebecca  alisema  polisi  zaidi  walifika  kwenye  eneo  hilo  wengine  wakiwa  kwenye  pikipiki  na  kuanza  kuwafukuza  majambazi  hao  ambapo  walipofika  eneo  la  shule  ya  St. Marry's,walitupa  kiroba  kimoja  cha  fedha  ambacho  wananchi  waliokuwa    jirani  waligombania  na  kuchukua  fedha  zilizokuwemo  na   kisha  kila  mmoja  kukimbia  na  burungutu  la  noti.

Baada  ya  nusu  saa  wakati  umati  ukiwa  bado  upo  kwenye  benki  hiyo,magari  ya  polisi  yalipita  katika eneo  hilo  yakitokea  eneo  la  Mkuranga  yakiwa  yamebeba  miili  ya  majambazi  yaliyouawa.

Magari  hayo  yalikuwa  yakisindikizwa  na  vijana  wa  bodaboda  waliokuwa  wakishangilia  kazi  iliyofanywa  na  polisi.

Kamanda  wa  polisi  kanda  maalum ya  Dar es Salaam, Simon Sirro  alizungumzia  kwa  ufupi  tukio  hilo n kwamba  majambazi  manne  yaliuawa  na  kukamata  silaha  tatu,lakini  hakutaka  kuingia  kwa  ndani  akisema  atatoa  taarifa  zaidi  leo

Top Ad 728x90