Top Ad 728x90

Tuesday, 1 March 2016

Mahiza Abaini Ufisadi Tanga..Sh36 Bilioni za Miradi 66 Zimetafunwa..Wapewa Siku 14


Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza amesema Sh36 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi 66 ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji Tanga, zimefujwa.

Mahiza alisema hayo juzi katika kikao cha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, makandarasi, wahandisi na wakurugenzi wa wilaya za Mkoa wa Tanga.

Alisema ni miradi 30 tu iliyotekelezwa huku mingine 36 ikiwa haijatekelezwa na fedha kutumika.

Mahiza alifanya kikao hicho baada ya kumaliza ziara yake ya siku 10 ya kukagua miradi ya maji mkoani humo na kubaini ufisadi huo.

“Nawapa siku 14 mniletee maelezo kwa nini msichukuliwe hatua kwa kufanya kazi isiyo na tija na kuonyesha uchu wa kutaka fedha za miradi hali mkijua hamuwezi kuitekeleza na kutoishauri Serikali kuhusu njia sahihi,” alisema.

Alisema makandarasi na wahandisi ambao hawakutekeleza miradi watakuwa chini ya uchunguzi wa maofisa wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Idara ya Usalama wa Taifa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Sh36 bilioni zimehujumiwa na wataalamu (watendaji) ambao hawaitakii mema Tanga, imenigusa, imeniumiza kupita kiasi, nimekasirika, haya ni majipu makubwa tutayatumbua bila ganzi.

“Mmetutengenezea fitina kati ya Serikali na wananchi,” alisema Mahiza.

Alisema baada ya kupokea maelezo hayo atakutana na kamati yake ya ulinzi na usalama kushauriana kisha majina yote ya waliohusika yatafikishwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa ajili ya uamuzi.

Mhandisi wa Maji Mkoa wa Tanga, Ephraim Minde alisema miradi hiyo 30 iliyokamilika ipo katika Wilaya za Korogwe, Lushoto, Kilindi na Tanga.

Mmoja wa wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Noel James alisema mradi wa umwagiliaji wa Mwakijembe Wilaya ya Mkinga unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

0 comments:

Post a Comment

Top Ad 728x90