- Wasema BMK lilikuwa sawa na Mkutano wa CCM na limetumia ujanja kupitisha Katiba
- Wajiandaa hatua za kuchukua, wataka Watanzania kukaa mguu sawa
SIKU moja baada ya Bunge Maalum la Katiba kupitisha Katiba inayopendekezwa, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ume
goma kutambua matokeo ya kura zilizopigwa kupitisha Katiba hiyo.
UKAWA ambao unaundwa na vyama vya Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), na NCCR-Mageuzi, wamekuwa wakifanya mashauriano na hatimaye kuueleza umma hatua itakazochukua.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano CHADEMA, ilisema kuwa viongozi wa CHADEMA wanaendelea na mashauriano na wenzao katika UKAWA, kupitia vikao vyao vya ndani.
“Baada ya vikao na mashauriano hayo, viongozi wa UKAWA watawaeleza Watanzania maana ya uharamia huo na watatoa msimamo dhidi ya uharamia uliofanywa na Bunge Maalum la Katiba,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bunge Maalum la Katiba limetumia njia za kiharamia kupata theluthi mbili ya kura za Zanzibar na kuwahadaa Watanzania kwamba kura hizo ni halali.
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa, BMK lilikuwa sawa na Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na limetumia njia za kiharamia kupitisha katiba hiyo inayopendekezwa.
Taarifa hiyo, imewataka Watanzania kutambua kuwa BMK limetangaza mgogoro na mwanya mwingine wa agenda kubwa ya kuwaunganisha Watanzania kupigania mabadiliko ya kweli dhidi ya maharamia wa demokrasisa na maoni ya wananchi.
“CHADEMA kama walivyo wenzao kupitia UKAWA, wanajua kuwa Watanzania katika wingi mkubwa ambao kiu yao ya Katiba Mpya na bora haijakidhiwa, badala yake wameongezewa uchungu, wana shauku kubwa kusikia maelezo, ufafanuzi wa uharamia uliofanyika Dodoma juzi na wasubiri kusikia maelekezo ya hatua itakazochukua,” ilisema taarifa hiyo.
Katika matokeo yaliyotangazwa juzi, Naibu Katibu wa Bunge Maalum, Dk. Thomas Kashilillah, alisema Bunge hilo lilikuwa na wajumbe 630, kati yao Wazanzibari ni 219 na kwamba, kati ya hao waliopiga kura ni 154 na ili kupata theluthi mbili ya Zanzibar, zilihitajika kura 146.
Kwa upande wa Bara, Dk. Kashilillah alisema wajumbe walikuwa 411 lakini waliopiga kura ni 335 na ili kupata theluthi mbili ilitakiwa kura za wajumbe 274.
Alisema kwa mujibu wa kura zilizopigwa, theluthi mbili ya Zanzibar ilipatikana kwa ibara zote 289 ambapo ilikuwa ikibadilika kati ya 146,147 na 148 wakati kwa upande wa Bara theluthi mbili ilikuwa ikibadilika kuanzia 332, 133 na 134 kutegemeana na ibara.
“Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe waliopiga kura za ndiyo za wazi ni kati ya 106 hadi 108, wajumbe kati ya 7 hadi 8 walipiga kura za hapana za wazi wakati kura za siri zilikuwa kati ya 38 hadi 40 ambazo zote zilikuwa za ndiyo isipokuwa moja tu ilikuwa ya hapana katika baadhi ya ibara,” alisema.
Kwa Bara, kura za ndiyo za wazi zilikuwa kati ya 301 hadi 304, kura ya wazi ya hapana ilikuwa kati ya moja hadi tatu, kura za siri za ndiyo zilikuwa kati ya 29 hadi 31 wakati kura za siri za hapana zilikuwa kati ya moja hadi mbili
0 comments:
Post a Comment