Top Ad 728x90

Sunday 5 October 2014

Kamanda Halima Mdee aandamana Dar.

  • Aongoza maandamano ya akina mama kwenda Ikulu
  • Atiwa mbaroni, akataa dhamana hadi atoke na wenzie
Halima Mdee akiongoza maandamano ya akina mama kwenda Ikulu
JESHI la Polisi jana lilitembeza mkong’oto na kuwakamata makada na
viongozi wa Baraza la Wanawake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), waliokuwa wakiandamana kwenda Ikulu
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee ni miongoni mwa viongozi walioonja shuruba ya polisi waliokuwa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam kuzuia   maandamano ya Bawacha
Wiki chache zilizopita Mdee, alitangaza baraza hilo kufanya maandamano ya amani kuelekea Ikulu, kumtaka Rais Kikwete asisaini katiba inayopendekezwa, iliyopitishwa wiki iliyopita na Bunge Maalum la Katiba.
Hata hivyo juzi Kamishna wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipiga marufuku maandamano hayo.
Hata hivyo jana Mdee aliwaambia waandishi wa habari maandamano hayo yana baraka za Rais Jakaya Kikwete, aliyemkaribisha Ikulu wakiwa katika uzinduzi wa barabara ya Mwenge -Tegeta.
Mdee alisema ni lazima aongoze maandamano hayo kwasababu ni haki yao kwa mujibu wa Katiba iliyopo sasa ibara ya 18 na 20 ambazo zinampa kila raia uhuru wa kuandamana, kujieleza na kusikilizwa.
“Mimi ni mwanasheria na mbunge wa nchi ambaye ninaielewa vizuri sheria ya nchi kwa kuwa ninaitunga… tuna kila sababu za kuandamana kutokana udhalimu unaofanywa kila siku na hatuwezi kukubali kukaa kimya huku taifa linateketea wakati sheria zinaturuhusu kufanya hivyo” alisema Mdee
Alisema alipata taarifa za kuzuiwa kwa maandamano yao juzi usiku ambapo alishindwa kuyasitisha kwakuwa taarifa ya Kova haikuwa na sababu za msingi
Mdee alisema maandamano hayo yalikuwa na malengo mengi kubwa zaidi ni kupinga Katiba iliyopendekezwa mwishoni mwa wiki
Purukushani
Askari kanzu, polisi na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakiwa kwenye magari na silaha za moto pamoja na mabomu ya machozi walikuwa wakiranda randa kwenye Ofisi za Makao Makuu ya CHADEMA yaliyopo Kinondoni.
Kwa mujibu wa wakazi wa Kinondoni, Polisi walifika katika maeneo ya Ofisi za Makao Makuu ya Mabaraza ya CHADEMA saa 12 alfajiri.
Walifika eneo hilo wakiwa na magari aina ya Land Rover (Defender) yasiyopungua sita yakiwa na askari polisi wa kike na kiume waliokuwa wamebeba bunduki na virungu
Askari hao pia waliambatana na gari kubwa lenye maji ya kuwasha tayari kwa kukabiliana na waandamanaji.
Majira ya saa nne, Mdee alifika nje ya ofisi hizo akiwa kwenye gari dogo, na  aliposhuka, wanawake waliokuwa eneo hilo walianza kumshangilia.
Mdee alikuwa akitoa kauli mbiu ya chama hicho na Bawacha ‘Peoples’ nao wakiitikia ‘power,’ ‘Wanawake’ wakiitikia ‘chimbuko la maendeleo’ kwa muda wa dakika 15.
Baada ya hapo aliingia ndani ya ofisi hizo kujua utaratibu wa maandamano kisha kuzungumza na waandishi wa habari.
Baada ya mazungumzo na waandishi wa habari Mdee, alitoka nje kuanza maandamano aliyoyaita ya amani kupitia barabara ya Kinondoni Makaburini, Selander Bridge hadi Ikulu.
Mara baada ya Mdee na makada wenzake kuanza maandamano hayo mita zisizopungua 70 kutoka ofisi za mabaraza, polisi waliwazuia.
Wakiwa katika eneo la karibu na makaburi ya juu ya Kinondoni, huku walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwemo ‘Rais usipochukua hatua, wananchi tutakulazimisha uchukue hatua.’
Polisi waliamua kumwagia waandamanaji maji ya kuwasha, baada ya kuwaamuru watawanyike, wakagoma. Hali hiyo ilizua taharuki na waandamanaji walikimbilia hovyo.
Halima Mdee ngangariKatika pilika pilika hiyo ya kukimbia Mdee aliingia katika kibanda cha wazi kilichoonekana ni mgahawa ambapo  askari wasiopungua sita walimfuata na kumpiga virungu. Yeye na na makada wenzake walipakiwa kwenye gari magari na kupelekwa kituo cha polisi.
Gari lililokuwa limewapatia wakina Mdee lilisindikizwa na magari mengine manne, huku lile gari la maji ya kuwasha na mengine yakiendelea kuimarisha ulinzi.
Baada ya magari hayo kuondoka kwa kasi taarifa zilisema amepelekwa kituo cha Polisi Oysterbay kuhojiwa.
Hali ya ulinzi katika kituo cha Oysterbay ulinzi ulikuwa umeimarishwa ambapo askari wenye bunduki, virungu na magari ya kuwasha walitanda.
Askari polisi walipoona wafuasi wa CHADEMA wanazidi kusogea katika viwanja vya kituo waliweka uzio wa kamba ya nailoni kuwazuia kuingia eneo hilo.
Baada ya kuzuiwa kuingia, wafuasi hao wa CHADEMA walivuka ng’ambo ya pili na kuendelea kuimba nyimbo mbalimbali huku wakililaani jeshi la polisi kutumiwa na CCM kuwadhibiti wapinzani.
Mwenyekiti huyo na wenzake wanane walishikiliwa kwa muda wa saa saba (kutoka saa tano hadi saa 11 jioni) kisha kuaachiwa kwa dhamana ya mdhamini mmoja mmoja kwa kila mmoja kwa masharti kwamba lazima wawe maofisa wa chama.
Ofisa Habari wa CHADEMA Tumaini Makene, alisema Mdee alikataa kuachiwa peke yake mpaka atoke na wenzake.
Baada kuachiwa walielekea jimboni kwake Kawe, Kata ya Bunju kwa ajili ya  mkutano wa hadhara, akatoa shukrani kwa wanawake waliomuunga mkono.
Waandishi kutoka vyombo mbalimbali  walizuiwa na polisi waliokuwa wakilinda katika kituo hicho cha Oysterbay, wakidai ni agizo maalumu.
“Hii ni oda kutoka kwa mkubwa, hakuna mtu yoyote wakuingia katika eneo hilo …na nyie waandishi nendeni huko, mkihitajika mtaarifiwa,” alisema askari aliyesomeka kwa jina E. M. Tille.

0 comments:

Post a Comment

Top Ad 728x90